Kusaidia kusomesha watoto yatima na wenye uhitaji katika jimbo la Bukoba ili kuwatayarisha waweze kuchangia katika kutatua changamoto za kiuchumi zinazokabili familia zao na jamii yao na kushiriki katika utume wa Kanisa kwa ajili ya wokovu wa watu.

Kauli Mbiu yetu
Ili Wawe na Uzima ambayo ni msingi wa shughuli zote za BUCADOS inatokana na maneno ya Bwana Wetu Yesu Kristo:
"Mimi nalikuja ili wawe na uzima" (Yohana 10:10). Tunatafsiri utume huu wa Kristu kuwa ndio utume wa Kanisa na kwa hakika ndio utume wa kila mbatizwa, kushiriki katika kazi ya wokovu; kujitoa kwa ajili ya maisha ya wengine. Maisha katika maana yake kamili yanajumuisha ustawi wa mtu kiroho (uzima wa milele) na kimwili (elimu, chakula na malazi). Hivyo basi, kumsomesha mtoto au mtu mwingine mwenye uhitaji, ni kuwaandalia msingi imara wa maisha; kuwapa uzima.
Kwa bahati mbaya, mara nyingi, yatima na watoto kutoka kwa familia zenye uhitaji hawapati msingi huu mzuri wa maisha kwa sababu hawana mtu wa kugharimia masomo yao ambayo kila mara yanazidi kuwa ghari sana. Kutokana na hali hii, na katika roho ya Kristu, ambaye
"aliwahurumia kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji" (Mt 9:36) na kwa kuongozwa na mafundisho yake
"Lolote mlilomtendea mmoja wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi" (Mt 25:40), Jimbo Katoliki la Bukoba lilianzisha shirika la BUCADOS ili kuwapa uzima watoto yatima na wahitaji kwa kuchangisha fedha ili kuwasomesha kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.
Tunachokifanya
- Kuomba na kuchangisha fedha kutoka kwa wafadhili binafsi na mashirika ili kusomesha watoto yatima na wahitaji jimboni Bukoba.
- Kuanzisha na kuendesha shughuli za kiuchumi ili kuongeza kwenye fedha zilizochangwa katika kusaidia elimu ya watoto yatima na wahitaji.
- Kutoa ushauri nasaha kwa yatima ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kisaikolojia zinazotokana na kufiwa na wazazi.
- Kuzisaidia familia za watoto yatima wanaosaidiwa na BUCADOS kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazowasaidia kujitegemea na kuwasaidia watoto wengine ambao hawasaidiwi na BUCADOS.
Ujumbe wa Askofu

Wapendwa Familia ya Mungu,
Uhumuhimu wa elimu katika maisha ya mtu na hasa yatima ni mkubwa sana. Mtakatifu Matayo anatwambia:
“Yesu aliwaonea huruma kwa kuwa walikuwa wamechoka na kudhoofika kama kondoo wasio na mchungaji” (Mt 9:36). Yatima wanapokosa fursa ya kusoma, wanatawanyika kama kondoo wasio na mchungaji na kuishia mitaani, wakiombaomba na kutumbukia katika uharifu, na kuwa wathirika wa madawa ya kulevya, kutumikishwa, unyanyasaji wa kijinsia na biashara ya binadamu. Jimbo Katoliki la Bukoba limekuwa kila mara mstari wa mbele katika kusaidia maskini wakiwemo yatima. Tunamshukuru Pd. Achilles Kiwanuka Macvhumilane kwa wazo la kuanzisha shirika la BUCADOS ili kusaidia kusomesha yatima. Nimetamani jambo hili siku nyingi kwa sababu mimi mwenyewe nilikuwa yatima, na hivyo nafahamu madhira wanayopitia yatima katika maisha yao. Kama methali isemavyo:
“Usimpatie mtu samaki bali mfundishe kuvua,” tunatumaini kuwa kupitia BUCADOS, yatima watapata elimu na ujuzi wanaohitaji ili kujitengenezea maisha yao ya baadaye na kushiriki katika maendeleo ya jamii yao. Kwenu nyote na kwa wale wote watakaoifahamu BUCADOS kupitia kwenu, nawatakia Baraka za Mwenyezi Mungu na kuwaalika kutuunga mkono kwa kuchangia chochote kidogo ulichonacho ili kuisaidia BUCADOS katika malengo yake na kwa pamoja tuweze kushiriki katika utume wa Bwana wetu Yesu Kristu kama asemavyo:
“Nimekuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yn 10:10); na kutimiza utume aliotuachia akisema
“waacheni watoto waje kwangu” (Mt.19:14). Mungu na awabariki.