Kuhusu BUCADOS

BUCADOS ni shirika la kusaidia kusomesha yatima na wahitaji linalofanya kazi zake chini ya Jimbo Katoliki la Bukoba mkoani Kagera, moja ya mikoa 31 ya Tanzania. Mkoa wa Kagera una ukubwa wa kilomita za mraba 35,686. Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya mwaka 2022, idadi ya wakazi wa Kagera inakadiriwa kufikia milioni 2.9, huku wengi wao wakiishi umaskini wa chini ya dola moja kwa siku. Kwa miongo kadhaa, Kagera imekuwa miongoni mwa mikoa yenye maendeleo duni nchini. Umaskini wa Kagera unachangiwa na ukweli kwamba sehemu kubwa ya mkoa huu ni vijiji, na uko mbali na bahari na mji mkuu, na kwa kiasi kikubwa wakazi wake ni wakulima wadogo wadogo.

Aidha, mkoa wa Kagera kihistoria umekumbwa na majanga ambayo yamesababisha familia nyingi kuwa yatima au kutumbukia katika umaskini wa mkubwa. Majanga haya ni kama, vita kati ya Tanzania na Uganda (1978-79), njaa kubwa na magonjwa kama UKIMWI ambayo yalizuka baada ya vita hivyo, kuzama kwa meli ya MV-Bukoba katika Ziwa Victoria (1996) na tetemeko la ardhi lililoukumba ukanda huu mwaka 2016. Haya yote yamechangia kudorora kwa uchumi wa eneo hili na kuziingiza familia nyingi kwenye umaskini zikishindwa kumudu elimu bora kwa watoto wao. Kwa hiyo, BUCADOS ina lenga kusaidia watoto yatima na watoto kutoka katika familia zisizo na uwezo kwa kufadhili karo na vifaa vingine vya elimu ili kupunguza mzigo kwa familia masikini na kuwatayarisha vijana kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya jamii ayo.


Kuhusu Mwanzilishi

Padre Achilles Kiwanuka Machumilane mwanzilishi wa BUCADOS ni padre wa Jimbo Katoliki la Bukoba nchini Tanzania aliyezaliwa na kukulia Bukoba. Akiwa na umri wa miaka 8, Pd Achilles na ndugu zake walikuwa yatima kufuatia kifo cha baba yao, Mzee Dominic Rutakulemberwa aliyewaacha mikononi mwa mama yao Bertha Banagwa ambaye alikuwa mke wa nyumbani tu bila kipato chochote cha kiuchumi. Miaka iliyofuata ilikuwa ya shida kubwa kwa Pd Achilles na familia. Hapa chini, Pd Achilles anatushirikisha mapito aliyopitia akiwa yatima ambayo ndiyo sababu iliyomfanya aanzishe BUCADOS.

Wazo la kuanzisha shirika la kusaidia watoto yatima na wahitaji lilitokana na matatizo ya kiuchumi niliyokumbana nayo utotoni na wakati wa masomo yangu kama yatima. Baba yangu alifariki mwaka 1990 nikiwa bado mdogo, hata kabla sijajiunga na seminari. Baba yangu, ambaye alikuwa mwalimu, ndiye pekee tuliyekuwa tukimtegemea kwa matunzo ya familia yenye watoto kumi. Kwa bahati mbaya, alipofariki, ndugu zangu wakubwa walikuwa bado wanasoma na hakuna hata mmoja aliyekuwa ameajiriwa. Mama alilazimika kubeba mzigo huu mzito peke yake. Kwa sababu hiyo, mimi na ndugu zangu tulikabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha wakati tukisoma. Nakumbuka ada na mahitaji mengine ya kujiunga na Seminari ya Rutabo yalichangiwa na waumini wa kigango chetu cha Nyakigando, Parokia ya Kishogo. Baadaye, kila nilipokuja likizo, nililazimika kutengeneza pombe ya kienyeji (rubisi) ambayo niliiuza ili kupata ada na mahitaji mengine ya shule. Nilipojiunga na Shule ya Sekondari katika Seminari ya Mt. Maria, Rubya hali ilikuwa ngumu zaidi. Mwanzoni mwa kila muhula, nilirudishwa nyumbani siku iliyofuata kwa sababu sikuwa na karo. Mama alijitahidi sana kunitafutia karo akiomba msaada kutoka wa watu mbalimbali. Kwa bahati nzuri, nilipokuwa kidato cha pili, rafiki mmoja alituelekeza kwenye shirika la Kilutheri liitwalo HUYAWA- Huduma YA Watoto, ambalo linasaidia watoto kutoka familia maskini. Walikubali ombi langu na kunifadhili karo kwa miaka mitatu hadi nilipomaliza kidato cha nne. Hii ilinigusa sana na nikatamani siku moja kuanzisha shirika kama hilo ili kuwasaidia watoto wengine ambao wana shida katika kupata karo.






Hata hivyo, kwa sababu hali yao kifedha, HUYAWA wanasaidia tu mpaka kidato cha nne. Hivyo, kwa kidato cha tano na sita ilibidi nitafute msaada sehemu nyingine. Nilibisha hodi huku na huko nikitafuta msaada, bila mafanikio. Hatimaye, nilimshirikisha hali yangu Baba Askofu Nestory Timanywa, Askofu wa Jimbo la Bukoba wakati ule, ambaye alinionea huruma na kunipa msamaha wa karo kwa kidato cha tano na sita. Bwana mwenye rehema ampokee katika amani yake ya milele.

Mahangaiko haya yaliniumiza lakini yalinipa hamu kubwa ya kusaidia yatima na maskini, kwa sababu ninaamini kwamba kuna yatima wengi ambao wako katika hali kama hiyo au hata ngumu zaidi. Tangu nilipopadrishwa, mwaka 2008, nimekuwa nikitumia kidogo ninachopata kusaidia kulipa karo za watoto wenye mahitaji. Hata hivyo, nia yangu ilikuwa ni kuanzisha shirika ambao lingeweza kuwasaidia watoto yatima kwa kiwango kikubwa, na kwa kushirikisha wafadhili wengi zaidi, lakini sikuweza kutimiza ndoto yangu kwa sababu nilikuwa nikiendelea na masomo yangu. Namshukuru sana Baba Askofu Jovitus Mwijage, Askofu wa sasa wa Jimbo Katoliki la Bukoba, kwa kulikubali wazo langu na kuahidi kunisaidia katika kutimiza ndoto yetu. Ni kutokana na juhudi zake, BUCADOS imeanza. Tunaomba wafadhili zaidi watuunge mkono katika juhudi zetu kwa kuchangia utume wa BUCADOS ili yatima wawe na uzima.




Lengo la Shirika

Kusaidia kusomesha yatima maskini na watoto wenye uhitaji jimboni Bukoba ili kuwaandaa kushiriki katika kutatua changamoto za kiuchumi.

Soma zaidi


Saidia

Tunakaribisha msaada wa kifedha kutoka kwa watu binafsi na mashirika, kupitia Bank Transfer, Credit Card na PayPal.


Soma zaidi


Jiunge Nasi

Unakaribishwa kujiunga na Marafiki wa BUCADOS ili usaidie kuchangia na kueneza lengo la BUCADOS ili kuwafikia wafadhili wengi zaidi.

Jiunge


Copyright © 2024 Bukoba Catholic Diocese - All Rights Reserved

Designed by Creative Mind